Anaandika Dauka Simba :
SERIKALI MUIKUMBUKE TIMU YA TAIFA YA NGUMI YA TANZANIA ILI KUIPA PONGEZI KWA HESHIMA WALIYOIWEKA PALE KENYA
Itakumbukwa kwa mara ya kwanza katika historia ya sekta ya michezo nchini Tanzania ilifanikiwa kuandika historia ugenini ambapo timu ya Taifa ya ngumi ya Tanzania maarufu kama Faru Weusi ilishinda medali 18 katika mashindano ya ngumi barani Afrika.
Tanzania ilifanikiwa kupata medali moja ya dhahabu, nne za fedha na za shaba 13 pia Tanzania ikashika nafasi ya nne katika mashindano hayo kitendo ambacho kilisababisha viongozi wakubwa wa vyama vya ngumi Duniani kuanza kuitolea macho Tanzania kwenye mchezo wa ngumi hasa kwa upande wa timu yetu ya Taifa ya Tanzania maarufu kama Faru Weusi.
Nilipokua pale Nairobi nilipata nafasi ya kuzungumza na wadau mbalimbali wa ngumi wakiwemo wanahabari wenzangu ambao walinihoji kuhusu ubora wa timu yetu ya Taifa ya ngumi pia baada ya mashindano hayo 'General' wa jeshi la Polisi wa serikali ya DR Congo aliialika timu ya Tanzania katika chakula cha jioni kutokana na kiwango bora walichokionesha kwenye mashindano yale.
Mnamo Oktoba 26 mwaka huu yaani siku mbili baada ya mashindano yale ya ngumi barani Afrika ambayo yalifanyika nchini Kenya, msemaji mkuu wa serikali Persona Msigwa akiongea na vyombo vya habari katika uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kumalizika kwa mchezo wa ligi ya mabingwa barani Afrika kati ya Simba SC dhidi ya Nsingizini Hotspurs aliipongeza timu ya Taifa ya ngumi ya Tanzania kwa kazi nzuri waliyoifanya huku akisema watawapongeza.
"Tunawapongeza sana tutaandaa utaratibu wa kukutana nao na kuwapongeza rasmi," alisema Msigwa.
Ni mwezi sasa umepita hakuna muendelezo wowote kuhusu kile ambacho serikali imessema kupitia msemaji wake, Msigwa lakini Desemba tatu mwaka huu tumeona serikali iliipongeza timu ya Taifa ya wanawake Twiga Stars kwa kuwapa milioni 50 baada ya kufuzu michuano ya WAFCON mara mbili mfululizo.
Ombi langu kwa serikali tusiishau timu yetu ya Taifa ya ngumi ya Tanzania ambao nao wamekua mstari wa mbele kuitangaza nchi yetu kwani nao wanastahili hizi pongezi kama walivyo wanamichezo wengine.

0 Comments