Klabu ya Yanga imetangaza Rasmi mshindi wa tenda ya ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo ambaye ni kampuni ya GSM TANZANIA LIMITED. Tangazo la ujenzi huo limetolewa na afisa habari wa klabu Ally Kamwe kupitia mkutano na waandishi wa habari uliofanyika 2 February 2026 katika ofisi za klabu.
Kamwe amenukuliwa akisema
“Siku ya Jumamosi uongozi wetu ulikaa kikao cha kamati ya Utendaji inayoongozwa na Rais Eng. Hersi Ally Said na kujadili agenda moja ya Msingi ya McLakato wa ujenzi wa uwanja wa Young Africans Sports Club, Kikao kile kilikwenda kutoa majibu ya kampuni au Taasisi iliyoshinda Tenda ya kushirikiana na Yanga kwenye ujenzi wa uwanja wa Yanga.
“Kabla hatujamtaja mshindi wa Tenda hii naomba niwapitishe kwenye mchakato mzima wa Ujenzi wa Uwanja huu, Mchakato huu umepita kwenye hatua mbali mbali, hatua ya kwanza ilikuwa kufanya Tathmini ya eneo la ujenzi wa uwanja, baadae tukagundua kuwa kuna Eneo la ziada linahitajika kwenye kukamilisha ujenzi huo, baadae tukashirikiana na Serikali kuomba eneo la ziada.
Hapa nichukue Fursa hii kuishukuru Serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia Eneo la ziada"
Viongozi wetu wakiongozwa na Rais wa Klabu walikuwa na ndoto ya kujenga uwanja, wakaamua kuwa uwanja ujengwe makao makuu ya klabu yetu. Wakashauriwa na wataalamu. Lakini wakagundua lazima wapate nyongeza ya ardhi ili uwanja wetu ukidhi matakwa CAF. Serikali ikatupatia eneo na Hati tunayo na baada ya mchakato huo tukatafuta mkandarasi ambaye atatujengea uwanja. Hatimaye GSM Tanzania LTD wameshinda tenda hii”
USHIRIKIANO WA KIMKAKATI BAINA YA YANGA NA GSM
Ushirikiano wa kibiashara baina ya Klabu ya Yanga na makampuni ya GSM umedumu kwa Miaka 6 na umekuwa ukileta matokeo chanya kwa Klabu hiyo.
Kampuni ya GSM imekuwa ikitengeneza na kusambaza jezi za klabu ya Yanga kwa kipindi cha miaka minne na wamekuwa wakitoa jezi zenye viwango vya kimataifa.
Kampuni ya GSM imekuwa ikiidhamini klabu ya Yanga kupitia bidhaa zake za vinywaji na Magodoro wanayozalisha na hata suala la bonasi kwa wachezaji pamoja usajili wa wachezaji wamekuwa wakihusika kuisaidia klabu hiyo
Ushirikiano baina ya taasisi hizi mbili umeleta mageuzi chanya ndani ya klabu na wananchi wameishuhudia timu Yao ikiwa tishio kwa Misimu minne mfululizo ikishinda makombe ya Ligi kuu,FA,Muungano,Mapinduzi na imegeuka timu tishio barani Afrika kwa kufika fainali za kombe la Shirikisho.
TUTEGEMEE UKAMILISHWAJI WA UWANJA KWA MUDA MUAFAKA
Kitendo cha uongozi wa Young Africans kuipa tenda ya ujenzi kampuni ya GSM ni dhahiri Jambo hilo linakwenda kutekelezwa kama walivyokubaliana na linakwenda kuipeleka Yanga kwenye viwango vipya na kuwa ni Moja ya klabu chache nchini zitakazomiliki viwanja vya kisasa .
Utekelezaji wa mikataba ambayo GSM wamekuwa wakisaini na Yanga imegeuka chachu kwa Uongozi wa Yanga kuipa tenda kampuni hiyo na pia uhakika wa kutokwama kwa mradi wa ujenzi kutokana na kampuni hiyo kuwa na msuli wa kifedha hivyo mambo yanakwenda kuwa mazuri Jangwani


0 Comments