Manchester City wamemtangaza rasmi Enzo Maresca kama meneja wao mpya huku Chelsea ikidai kuwa Muitaliano huyo atalipa fidia binafsi kama sehemu ya suluhu itakayomruhusu kuchukua mikoba katika uwanja wa Etihad.
Hatimaye Maresca alitambulishwa kama mrithi wa Pep Guardiola kwa mkataba wa miaka mitatu Jumatatu.
Tangazo hilo lilifuatiwa haraka na taarifa ndefu kutoka kwa Chelsea ambapo klabu hiyo ilisema wamepokea fidia kutoka kwa City na Maresca mwenyewe.
Katika taarifa yake kwenye mtandao wa Instagram, Maresca aliomba radhi kwa Chelsea kwa "usumbufu" uliosababishwa na kuondoka kwake Stamford Bridge mnamo Januari, lakini alisema "amefurahishwa" kujiunga na City.
Vyanzo vilivyo karibu na City vimeiambia amospoti kwamba uhusiano wao na Chelsea unasalia kuwa mzuri na kwamba kuchelewa kumtangaza Maresca kulitokana na mzozo wa kimkataba kati ya kocha huyo mwenye umri wa miaka 46 na Chelsea.
Taarifa ya Chelsea ilisema: "Mnamo msimu wa vuli mwaka jana, klabu iliarifiwa na kocha wetu mkuu wa zamani kwamba huenda kukawa na nafasi ya kumrithi Pep Guardiola mwishoni mwa msimu.
“Ilitudhihirikia kuwa ni hamu yake kubwa ya kutaka kumrithi Guardiola na kwamba alikuwa amejitolea kabisa kutafuta nafasi hiyo, licha ya kwamba alikuwa chini ya mkataba wa muda mrefu ambao hakuwa na haki ya kuuvunja.
"Mnamo Desemba 2025, kocha wetu mkuu bila kutarajia na ghafla alijiuzulu wadhifa wake.
"Katika mazingira na kwa kuzingatia heshima kati ya vilabu, suluhu ya siri imefikiwa na Manchester City, ambayo ni pamoja na malipo ya fidia.
"Maamuzi ya siri pia yamefikiwa na aliyekuwa Kocha Mkuu ambapo atalipa fidia."
Maresca alijiunga na Chelsea mwaka wa 2024 kwa mkataba wa miaka mitano na alishinda Kombe la Ligi na Kombe la Dunia la Vilabu kwa muda wa miezi 18.
Aliondoka Stamford Bridge mnamo Januari 1, 2026 na nafasi yake ikachukuliwa na Liam Rosenior. Baada ya kipindi kibaya cha pili cha msimu, Rosenior alitimuliwa mwezi Aprili huku Chelsea ikimaliza katika nafasi ya 10 kwenye Ligi Kuu ya Uingereza na kukosa kufuzu kwa Uropa.
Maresca anarejea City kwa kipindi cha tatu baada ya hapo awali kufanya kazi kama kocha mkuu wa Kikosi cha Kukuza vijana na kama msaidizi wa kikosi cha kwanza cha Guardiola kati ya 2022 na 2023.
"Mwishoni mwa Desemba 2025, nilifanya uamuzi mgumu kuondoka Chelsea," Maresca alisema katika chapisho kwenye Instagram.
"Uamuzi ulikuwa wangu tu. Kujiuzulu kwangu kutoka Chelsea kulinifungulia njia ya kujiunga na Manchester City, ambayo ni klabu niliyokuwa naifahamu vyema. Nina furaha kwamba sasa nimejiunga na Manchester City.
"Ninatambua kwamba kuondoka kwangu Chelsea katikati ya msimu kulisababisha usumbufu kwa klabu na naomba radhi kwa hilo. Haikuwa nia yangu wala matakwa yangu."

0 Comments